S H E I K H

l o a d i n g

About Sheikh


WASIFU WA SHEIKH ABDILAHI NASSIR

 

Utangulizi

Sheikh Abdilahi Nassir, aliyezaliwa Mombasa, Kenya, tarehe 1 Juni, 1932, alikuwa ni miongoni mwa wanachuoni wakubwa wa madhehebu ya Ahlul-Bayt. Baba yake ni Nassir bin Juma; na mamake ni Maryam binti Ahmad. Chimbuko lake linatokana na madhehebu ya Sunni, lakini alijitangaza hadharani kuwa mfuasi wa Maimamu 12 baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, yaliyotokea mwaka 1979.

 

Maisha Yake ya Utotoni na Elimu

Alipofika umri wa miaka mine, Sheikh Abdilahi alipelekwa chuoni (madrasa) kusomeshwa Qur’ani. Baina ya mwaka 1941 na 1949 alipata elimu ya msingi, mpaka darasa la sita, katika shule iliyoitwa Arab Boys Primary School, Mombasa. Kuanzia mwaka 1950 alisomea ualimu kwa miaka miwili katika Chuo cha Ualimu kilichoitwa Teacher Training School, Zanzibar, ambapo alihitimu masomo yake. Masomo aliyosomea katika Chuo hicho yalikuwa ni Kiswahili, Kiarabu na Dini*, Kiingereza, Historia*. Jiografia*, Hisabati, Misingi ya Elimu, Elimu ya Maumbile, Sanaa*, na Kazi za Ufundi. Katka mitihani ya masomo hayo mara kwa mara alikuwa akitokeza kushika nafasi ya kwanza; na katika mtihani wake wa mwisho alipata alama za juu kabisa katika masomo yaliyotiwa * hapa juu.


Huko Zanzibar, mbali na masomo yake ya ualimu, pia alitumia muda wake mwingi kujifunza na kupata mwongozo kwenye maarifa mbalimbali yahusianayo na Uislamu, kutoka kwa Sayyid Omar Abdallah, ambaye alikuwa ni miongoni mwa wanachuoni wakubwa wa wakati huo Zanzibar. Baada ya kuhitimu masomo yake Zanzibar, alirejea Mombasa. Hata hivyo aliendelea kushikamana, na mwalimu wake huyo, ambaye alikuwa chachu kubwa ya Sheikh Abdilahi Nassir kuuelewa zaidi Uislamu.


Aliporudi Mombasa, Sheikh Abdilahi alipata mwanachuoni mwingine kwao Kenya, Sheikh Muhammad Abdallah Ghazali, ambaye – kama Sheikh Abdilahi mwenyewe alivyokuwa akisema mara kwa mara - pamoja na mambo mingine, mwalimu wake huyo alimfundisha namna ya kutafakari mambo kwa kina, na pia kumshajiisha kuendelea kushikilia msimamo wake – almuradi tu awe anazo hoja thabiti za kuamini analoliamini.

 

Kazi Alizofanya

Punde tu aliporejea Mombasa, Sheikh Abdilahi alisomesha, kuanzia 1952 mpaka 1955, katika ile ile shule ya msingi aliyosomea utotoni  mwake, yaani Arab Boys Primary School. Baada ya hapo  akafanya kazi ya ukarani Mombasa Institute of Muslim Education (Taasisi ya Elimu ya Kiislamu Mombasa, ambayo ikijulikana zaidi kwa jina la MIOME, ambalo ni ufupisho wa jina lake kwa Kiingereza ) mpaka mwaka 1957, na wakati huo huo akisomesha elimu ya dini katika Taasisi hiyo.


Katika ujana wake, Sheikh Abdilahi alivutiwa na harakati za kisiasa za kupigania uhuru wa Kenya kutoka ukoloni wa Uingereza. Aliwahi kushika nyadhifa za uongozi katika vyama mbalimbali vya kijamii, kwa mfano Afro-Asian Association, ambapo mwaka 1958 alichaguliwa kuwa Makamu wa Katibu Mkuu; vyama vya kitamaduni na vya kueneza elimu (Coast Muslim Youth Cultural Society), na pia alishika nafasi za uongozi katika baadhi ya vyama vilivyokuwa vikipigania uhuru. Kwa mfano, katika ile miaka ambapo serikali ya kikoloni haikuwaruhusu Waafrika kuunda vyama vya kisiasa vya kitaifa, bali iliruhusu vyama vya maeneo ya miji au ya wilaya tu, Sheikh Abdilahi  alichaguliwa na chama kilichoitwa Mombasa Freedom Convention Party kushika wadhifa wa Katibu Mipango; halafu akawa ni miongoni mwa viongozi wa chama cha Coast Peoples Party, kilichokuwa kikipigania Mwambao wa Pwani ya Kenya; na mwaka 1960 alikuwa mwanachama mwanzilishi wa chama cha kitaifa cha Kenya African National Union (KANU), ambapo alichaguliwa kuwa Katibu Mwenezi katika Tawi la Mombasa.


Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1961 Sheikh Abdilahi alichaguliwa kuwa Mbunge katika Legislative Council (Baraza la Kutunga Sheria), akiwakilisha eneo bunge la Mombasa ya Kati (Mombasa Central). Alikuwa ni miongoni mwa wawakilishi walioshiriki  kwenye mkutano wa kuunda katiba ya Kenya kabla ya uhuru, uliofanyika Lancaster House, London, Uingereza, mwaka 1962 na 1963 - hatua ambayo iliifungulia njia Kenya kupata uhuru wake tarehe 12 Disemba, 1963.


Sheikh Abdilahi aliendelea kushika nafasi mbalimbali za kisiasa - hususani za kiushauri - katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru wa Kenya. Lakini miaka michache baadaye, hasa baada ya kuona jinsi siasa za Kenya huru zilivyokuwa zinakwenda kinyume na malengo yaliyokubaliwa wakati wa kupigania uhuru, Sheikh Abdilahi akapunguza sana shughuli zake za kisiasa na akawa anajishughulisha zaidi na kazi za tablighi, kutokana na kuamini kwamba mafunzo ya Uislamu ndiyo, hatimaye, yatakayowakomboa Wakenya – Waislamu na wasiokuwa Waislamu.


Baina ya mwaka 1965 na 1967 alifanya kazi katika Kituo cha Kusikilizia Habari (Monitoring Unit) cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mjini Nairobi, kwenye kitengo cha tafsiri cha lugha za Kiswahili na Kiarabu.


Kuanzia mwaka 1967 mpaka 1975 aliajiriwa kuwa Mhariri wa Kiswahili katika tawi la Afrika ya Mashariki la shirika la uchapishaji vitabu la Oxford University Press, Nairobi. Mbali na idadi kubwa ya vitabu alivyovihariri, na ambavyo baadhi yavyo vilitumika kusomeshea katika shule na vyuo vikuu vya Kenya na Tanzania, pia alivihariri vitabu vya Kiswahili vilivyoandikwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, vilivyochapishwa na shirika hilo la Oxford.


Mwaka 1975 Sheikh Abdilahi aliacha kazi Oxford University Press na akaanzisha shirika lake mwenyewe la uchapishaji vitabu, lililoitwa Shungwaya Publishers Limited. Miongoni mwa vitabu kadhaa vilivyochapishwa na shirika lake hili ni mijalada miwili ya Tafsiri ya Qur’ani Tukufu, Sura Al-Faatihah - Al-Baqarah na Sura Aali Imraan - An-Nisaa, za Sheikh Al-Amin bin Ali Mazrui; na tafsiri ya Sheikh Abdilahi Nassir ya Sura At-Talaaq.   

 

Mwaka 1977 shirika la Oxford University Press lilimwomba Sheikh Abdilahi arudi kufanya kazi nalo katika wadhifa mpya wa Meneja Mkuu wa tawi la Mashariki ya Afrika.  Aliushika wadhifa huo mpaka mwaka 1980 alipojiuzulu, ili awe na nafasi ya kushughulikia zaidi kazi za tablighi.

 

Kazi za Tabligh

Miongoni mwa kazi nyingi za tablighi alizoshughulika nazo Sheikh Abdilahi ni darsa za tafsiri ya Qur’an, hasa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Alianza darsa hizo katika mwaka 1960 kwenye Msikiti wa Shibu, ulioko eneo la Mwembe Tayari, Mombasa, na akaendelea nazo hapo mpaka mwaka1964. Alipohamia Nairobi mwaka 1965 akaendelea na darsa hizo za tafsiri ya Qur’an kwenye Masjid Riyadhwa (ambao unajulikana zaidi kwa jina la Msikiti wa Majengo, au Msikiti wa Pumwani). Mbali na darsa za tafsiri ya Qur’an, vile vile kila mwisho wa wiki alikuwa akisomesha darsa za Misingi ya Uislamu, ambazo zilikusudiwa maalumu kwa ajili ya vijana wanaume na wanawake, ingawa zikihudhuriwa na watu wazima pia. Aliendelea na shughuli hizo hapo Nairobi mpaka mwaka 1983 aliporudi Mombasa.


Kama ilivyoelezwa kabla, Sheikh Abdilahi aliingia katika madhehebu ya Ahlul Bayt baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979. Lakini hakufanya hivyo kwa kufuata mkumbo, bali aliyasoma, akayatafiti na kuyadadisi madhehebu haya kwa miaka mingi kabla ya kutangaza hadharani kwamba amekuwa mfuasi wa itikadi ya Shia Ithna-Ashari. Kwa hivyo, aliporejea Mombasa kutoka Nairobi mwanzoni mwa miaka ya ‘80 Sheikh Abdilahi alikuwa ni miongoni mwa wazungumzaji wakuu mashuhuri kwenye majlisi mbalimbali zilizoandaliwa na Bilal Muslim Mission of Kenya, na mihadhara yake iliwavutia wengi kutokana na aina yake ya uwasilishaji. Tangu wakati huo akawa anaendelea kufanya shughuli mbalimbali za kidini, kwa mfano kwa kushirikiana na WIPAHS (World Islamic Propagation and Humanitarian Services), Tanzania, Bilal Muslim Mission of Kenya, Bilal Muslim Mission of Tanzania na Al-Itrah Foundation. Kazi hizo ni pamoja na kurekodi video za darsa na mihadhara yake, na pia uchapishaji wa vitabu kadha wa kadha alivyoviandika kwa Kiswahili kuhusu maudhui mbalimbali yahusianayo na madhehebu ya Shia Ithna-Ashari, ambavyo vimeorodheshwa katika tovuti hii. Baadhi ya kazi hizo zimetarjumiwa kwa lugha za Kiingereza na Kinyarwanda.


Mbali na darsa na mihadhara aliyokuwa akitoa Kenya, Sheikh Abdilahi alipata kualikwa kutoa mihadhara katika nchi mbalimbali kwa lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu. Miongoni mwa nchi hizo ni Tanzania, India, Pakistan, Uingereza, Marekani na Kanada.


Mnamo mwaka 2001, Sheikh Abdilahi alianzisha taasisi ya Ahlul Bayt Centre, Mombasa, ambayo malengo yake makuu ni kuunganisha, kuhamasisha na kuelimisha watu kuhusu maswala mbalimbali yaliyofungamana na Uislamu, na pia kutoa huduma kwa jamii. Taasisi hiyo inaendelea kufanya kazi zake hizo.

 

 

Tuzo

Tarehe 22 December, 2006, Sheikh Abdilahi alikuwa ni miongoni mwa watu 17 waliotunukiwa tuzo ya heshima ya Freedom of the City of Nairobi. Tuzo hiyo ilitolewa kwa wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria waliohudhuria mkutano wa kuunda katiba ya Kenya, kabla ya Kenya kupata uhuru, uliofanyika London, Uingereza, mwaka 1962. Na Aprili, 2011, wakati wa Mkutano mkuu wa 72 wa Africa Federation uliofanyika Mombasa, Kenya, Mwenyekiti wa wakati huo, Alhaj Anwarali Dharamsi, alimtunuku Sheikh Abdilahi Nassir Tuzo ya Heshima ya Abbasi kwa kutambua utumishi wake na kujitolea kwake katika kueneza ujumbe wa Ahlul Bayt. 

 

Watoto Wake

Stambuli Abdilahi, Abdulqadir Abdilahi, Zainab Abdilahi, Nassir Abdilahi, Omar Abdilahi, Ali Abdilahi, Hafswa Abdilahi, Rehema Abdilahi, Sharifa Abdilahi na Hussein Abdilahi.                                   

 

Kifo chake

Sheikh Abdilahi Nassir alifariki dunia Mombasa, Kenya, alfajiri ya tarehe 11 Januari, 2022, akiwa na umri wa miaka 89. Alizikwa katika Maziyara ya Wakilindini, Ganjoni, Mombasa, Kenya. Kifo chake kiliombolezwa kwenye nchi mbalimbali duniani, zikiwemo Kenya, Tanzania (Bara), Zanzibar, Indonesia, Iran, Uingereza na kwengineko.